Kwa Jina La Allah Mwingi Wa Rehma Mwenye Kurehemu.

Sifa zote njema ni za Allah, na rehema na amani ziwe juu ya Mtume wake, na ziwe kwa wale wenye kumuiga na kumfuata mpaka siku ya Malipo.

Kwa hakika Qur’an tukufu ni muujiza wa kudumu ambao Allah ameuteremsha kwa Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake, na Allah akamuamrisha mtume wake kuufikisha kwa watu wote, na sisi tumeamrishwa kufikisha, kwa kauli yake Mtume rehema na amani ziwe juu yake: “Nifikishieni walau Aya moja tu”. Pamoja na kuwa Qur’an imeshushwa kwa lugha ya kiarabu, hakika tumeruhusiwa kutafsiri maana ya Qur'aan na kusherehesha maana yake, au kuisherehesha kwa lugha nyingine, ili ujumbe wa Allah ufike kwa watu wote.

Hivyo basi waislam wakaelekea kutafsiri maana ya Qur’an kwa lugha za ulimwengu, na hawezi yeyote kuitafsiri quraan kwa herufi, kwasababu ya lugha ya kiarabu na nduo lugha ya Quraan, ambayo Allah aliwapa changamoto waarabu walete mfano wake lakini walishindwa ingawa niwajuzi wa lugha ya kiarabu.

Walijaribu waisilamu na wengineo kutafsiri maana ya Qur’an tangu zama za muda mrefu, isipokua tafsiri nyingi katika hizo zimekengeushwa, au ni dhaifu, au ibara zake zinatokana na mtu mmoja pekee, au kundi la wengi walioshirikiana kati yao katika tafsiri bila ya kuwa na mfumo maalumu ulio wazi, na yote hayo yalipelekea kuwepo makosa na upotoshaji na udhaifu katika kunukuu ujumbe sahihi ambao Allah ameuweka katika Qur’ani tukufu.

Hivyo basi tukaanzisha Nuur International. Nacho ni kituo maalumu kinachojihusisha na kutafsiri Qur’ani tukufu kwa lugha mbali mbali za ulimwengu, kituo kinategemea mfumo wa kitaaluma katika kuchagua timu ya watendaji na kujikita katika mambo matano ya msingi, ambapo tafsiri inaanza kwa mfasiri mmoja mwenye sifa maalumu, kisha anairejea baada yake mtaalamu mwengine maarifa mapana ya uislam, kisha baada ya wao kurejea na kuipitia anafuata mbobezi mwengine katika upande wa lugha, kisha kunakuwa na jopo la majaji kutoka wenye vitivo tofauti tofauti, ili kuhukumu kazi katika ngazi zote, pamoja na kuipitia kila mmoja kazi ya mwenzake ili kuiboresha tafsiri vizuri, na yote hayo yapo chini ya usimamizi wa kitengo cha kitaaluma na wasimamizi ni madokta wenye fani mbalimbali.

Ama mfumo wa kutafsiri kwa ufupi upo katika nukta zifuatazo nazo ni:

1. Kulazimika katika kutafsiri Qur’an neno kwa neno bila ya kuzidisha au kupunguza, isipokua katika hali ambayo itakuwa ibara yenye kutafsiriwa si yenye kufahamika na inahitaji ufafanuzi zaidi, wakati huo basi kuifanyia kazi ibara hiyo itakua kwa njia mbili:

A- Itakapokua ziada ni neno moja au mawili inaweza kuongezwa pamoja na ibara ya husika kwa kuweka mabano mawili kama hivi: [ ]

B- Itakapo kuwa ufafanuzi ni mrefu itaongezwa (haamishi) upande wa chini katika kuandika ufafanuzi.

2. Kutegemea kufahamu maana sahihi kutoka katika hadithi za Mtume rehema na amani ziwe juu yake, na kauli za Maswahaba na wanachuoni wakubwa..

3. Kurejeaa katika tafsiri muhimu kwa ajili ya kufahamu maana ya ndani, mfano wa tafsiri ya Twabary, na tafsiri ya Ibnu Kathiri, na tafsiri ya Qurtubiy, na vilevile vitabu mahususi kwa kubainisha undani wa maarifa ya Qur’an.

4. Kuto kutafsiri jina la Mola (Allah) bali liandikwe kwa sauti kama linavyo tamkwa katika lugha husika, na tumebainisha sababu katika hashiya namba (1).

5. Kuthibitisha maana ya sifa za Allah kama vile ilivyokuja katika Qur’an tukufu bila ya kuzipotosha, na ni wajibu kwa msomaji afahamu ya kuwa sifa za Allah mfano mkono na sikio na jicho na kustawi juu ya kiti cha enzi na nguvu na sifa nyenginezo, na hata ikiwa katika tamko kuna mfanano wa sifa za Allah na viumbe lakini uhakika wake unatofautiana wazi kabisa; kwa mfano ukisema: Allah ana mkono, nikweli lakini sio kama mkono wa viumbe, na wala hatujui ulivyo mkono wa Allah mtukufu, na vivyo hivyo sifa zake zote tukufu, na katika mambo ya lazima katika itikadi ya kiislamu ni kuamini sifa za Allah zote, na kuzithibitisha kama zilivyo bila ya kuwaza, au kufananisha au kubadilisha maana, Allah Mtukufu anasema katika Aya 11 ya Surat Shuura: (Hana mfano wa chochote naye ni msikivu na mwenye kuona).

6. Kuchunga utaratibu wa Qur’an kisentensi katika kutanguliza na kuchelewesha ikiwa kanuni za lugha ya Kiswahili zinaruhusu Katika sifa za tafsiri na huduma zinazo tolewa kwa msomaji:

1. Kutumia lugha nyepesi iliyowepesishwa ambayo inawafaa wasomaji wote pamoja na kulindai fasihi na balagha ya lugha.

2. Nyongeza chache katika mabano na haamishi ili ipatikane ladha ya usomaji bila ya kupunguza maana.

3. Tafsiri inamsifu Allah Muumba mtukufu kama alivyo jisifu yeye mwenyewe binafsi, ili msomaji amjue Muumba ambae amemuumba na kuumba ulimwengu wote na vipi amuabudu kwa njia iliyo sahihi..

4. Inambainishia msomaji lengo la kuishi kwake na vipi aishi kwa njia iliyo sahihi, kama inavyo mbainishia mwisho wa matendo yake duniani na baada ya kufa kwake.

5. Mwisho kutilia umuhimu uandishi mzuri na ukubwa wake vivyo hivyo kuiandaa na kupangilia na kuchapisha; kwasababu uzuri wa umbo la tafsiri ni sehemu ya uzuri wa maudhui vilevile.

Na sisi wakati tunaweka tafsiri hii mbele yako ndugu msomaji, Tukitaraji kwa Allah iwe ni yenye manufaa kwako, na ikupe fahamu ya wazi katika ujumbe wa Allah aliyemtukufu, na kukusaidia kuufahamu uislamu, na kutenda yale yaliyo ya kheri, pamoja na tunakuzindua kua kwa kuifahamu Qur’an fahamu ya undani zaidi, ni lazima uisome kwa lugha ya kiarabu; hivyo basi tunamnasihi kila muislamu au anaetaka kujua uislamu sahihi, ajifundishe lugha ya kiarabu, nayo ni lugha nzuri na nyepesi kujifunza.

Mwisho kabisa tunaelekeza shukrani nyingi kwa kila alie changia katika hii tafsiri na kufanikiwa kwake na hasa hasa Profesa Zaydu bin Umar Al-Ayswi; Mkurugenzi wa taasisi ya kimataifa ya Bayyinaat Center for Qur'anic Studies, kama tunavyoishukuru pia timu ya wasimamizi na wahariri na kila alie changia katika kusambaza kazi hii kwa watu.

Na kila sifa njema anastahiki Allah Mola wa viumbe wote.

<